Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB YATOA ELIMU YA UFUGAJI BORA WA KISASA SHAMBA LA NG’OMBE WA MAZIWA HOMBOLO
19 Jan, 2024
TDB YATOA ELIMU YA UFUGAJI BORA WA KISASA SHAMBA LA NG’OMBE WA MAZIWA HOMBOLO

•      Yamuunganisha na wasindikaji na wafanyabiasha  wa maziwa

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) hivi karibuni imefanya ziara katika shamba la ng’ombe wa maziwa (Hombolo Farm) lililopo jiji la Dodoma na kutoa elimu ya ufugaji wa ng’ombe wa kisasa wa maziwa ili kuongeza uzalishaji  na kumuunganisha na soko la wanunuzi wa maziwa. 

Katika ziara hiyo, TDB ilifundisha mbinu mbalimbali za ufugaji wa kisasa na kibiashara unaozingatia kanuni bora za uzalishaji wa malisho na utengenezaji wa chakula cha ziada kitachopelekea kuongeza  uzalishaji wa maziwa ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida zaidi kwa kutumia malighafi yanayopatikana katika mazingira yanayomzunguka.

Aidha, katika ziara hiyo TDB ilisisitiza uongozi wa shamba kununua ng'ombe wa maziwa kwenye mashamba yanayozalisha ng’ombe bora wa maziwa ili kumpa mnunuzi taarifa sahihi na za kina kabla hajanunua. Hii itasaidia kupata ng'ombe sahihi na waliokusudiwa na kupunguza uwezekano wa kupata ng'ombe dhaifu au wenye uzalishaji mdogo.

Sambamba na hilo, Bodi imeahidi kushirikiana na mmiliki wa Shamba la maziwa la Hombolo katika kumuunganisha na  wanunuzi wa maziwa ambao watakubali kuingia mikataba rafiki kwa kuuza na kununua maziwa wakati wote wa mwaka.

Mtekinolojia Chakula Bw. Israel Mwingira kwa niaba ya TDB amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na shamba hilo za kuandaa malisho bora kama ilivyoshauriwa ambapo takribani hekari 13 za malisho aina ya Mtama malisho, Junkao, Brakaria na Napia zimelimwa na kuoteshwa ili kutatua changamoto ya chakula cha ng'ombe hususani wakati wa kiangazi.

Kwa upande wake mmiliki wa shamba hilo Bw. Benjamini Ndaki ameishukuru Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kumtembelea na kumpatia elimu muhimu katika uendeshaji wa shamba hilo la maziwa, amesema kuwa elimu aliyoipata itamsaidia kuongeza ufanisi na uzalishaji wa maziwa kwa wingi.