Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUHAMASISHA UNYWAJI MAZIWA HOSPITALINI
21 Jun, 2023
TDB YAADHIMISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA KWA KUHAMASISHA UNYWAJI MAZIWA HOSPITALINI

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Juni 20, 2023 imeungana na taasisi nyingine za serikali katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea na kuhamasisha unywaji wa maziwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma ambapo iligawa maziwa kwa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo wapatao 350.

Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa TDB, Meneja Utawala na Fedha Bw. Aggrey Msemwa amesema kuwa TDB imeona vyema kuja kuwatembelea wagonjwa na kuwapa maziwa ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ikiamini kuwa ili Taifa liweze kusonga mbele ni laziwa watu wake wawe na afya imara ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kila siku katika kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja hata kwa Taifa kwa ujumla.

“Katika Utumishi Umma afya ya mtumishi ni jambo la msingi sana ili aweze kutekeleza kwa weledi kazi anazopewa hivyo tumeona ni vyema tunapoadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma kuja kuwatembelea ndugu zetu ambao wamelazwa hapa hospitalini tukiamini kuwa miongoni mwa wagonjwa hawa wapo na watumishi wenzetu au familia zao ambao ni wagonjwa hivyo kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kujenga uchumi wa nchi kwa wakati huu ndio maana tukaona vyema tuje hapa na kufanya tendo hili dogo ikiwa ni sehemu ya utumishi wetu” Amesema Bw. Msemwa

Kaimu Muuguzi Mfawidhi wa hospitali hiyo Bi. Patricia Kabendera ametoa shukrani kwa Bodi ya Maziwa Tanzania  kwa kutembelea hospitali na kugawa maziwa kwa wagonjwa,  Pia ameihamasisha jamii kutumia maziwa kwani unywaji wa maziwa unasaidia kuleta afya ya mwili.

"Kama tunavyojua maziwa yana virutubisho mbalimbali ambavyo vinasaidia kwenye mwili wa binadamu. Maziwa pia ni chakula kilichokamilika ndio maana hata kwa mtoto mchanga maziwa ya mama peke yake huwa yanatosha bila kuhitaji Kitu kingine" Alisema Kabendera.

Kwa upande wake mgonjwa wa hospitali hiyo Bi.Jane Noeli Mgogoli ameishukuru Bodi hiyo kwa kugawa maziwa kwa wagonjwa kwani yatawasaidia wao kupata virutubisho ambavyo vitaenda kujenga mwili wao.