Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
TDB KUSHIRIKIANA NA MAAFISA LISHE KUHAMASISHA MATUMIZI YA MAZIWA KWA LISHE ZA WANAFUNZI NCHINI
30 Jun, 2023
TDB KUSHIRIKIANA NA MAAFISA LISHE KUHAMASISHA MATUMIZI YA MAZIWA KWA LISHE ZA WANAFUNZI NCHINI

Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imedhamiria kushirikiana na Maafisa Lishe nchini katika kuhamasisha na kutoa elimu juu ya  umuhimu wa matumizi ya maziwa kwenye lishe za wanafunzi ili kuimarisha afya zao na kuwakinga na maradhi ya mara kwa mara hali itakayosaidia kumudu masomo yao na kuongeza ufaulu hapa nchini.

Hayo yamesemwa Juni 28, 2023 na Kaimu Meneja Masoko wa Bodi ya Maziwa Tanzania Bw. Joseph Semu alipokaribishwa kuongea na Maafisa Lishe hao walioshiriki Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Lishe toka Tanzania Bara uliofanyika kwa siku mbili mfululizo katika Ukumbi wa Hoteli ya Dodoma Jiji uliopo katika Mji wa Kiserikali Mtumba.

Sanjari na hilo Bw. Semu amewataka maafisa hao kushirikiana na TDB katika kutoa elimu ya umuhimu wa kurasimisha sekta ya maziwa katika Halmashauri zao wanakotoka ili kuifanya sekta ya maziwa kuchangia katika pato la taifa.

Vilevile ameleeza kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Bodi ya Maziwa nchini ikishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wameshaandaa Mpango wa Unywjaji Maziwa Shuleni ambao utatekelezwa katika shule zote za Tanzania Bara, hivyo amewaomba kuwa karibu na kamati za chakula za shule zilizoko katika Halmashauri zao ili kuwajengea uwezo wa elimu ya lishe kwa watoto na maziwa yakiwa sehemu ya lishe.

Bodi ya Maziwa Tanzania imeshiriki kikao hicho kama mdau mkubwa wa mambo ya lishe hapa nchini hasa katika kuhamasisha matumizi ya maziwa yaliyosindikwa ili kuinua kipato cha mfugaji mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.