Bodi ya Maziwa Tanzania
Wizara ya Mifugo na Uvuvi

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,

TDB Logo
ASAS YAZINDUA KAMPENI YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI VISIWANI ZANZIBAR
28 Aug, 2023
ASAS YAZINDUA KAMPENI YA UNYWAJI MAZIWA SHULENI VISIWANI ZANZIBAR

Kampuni ya ASAS Dairies Agosti 26, 2023 imezindua kampeni ya Unywaji Maziwa Shuleni Visiwani Zanzibar mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ambaye ameonesha kufurahishwa na kampeni hiyo wakati akifungua rasmi tamasha la Kizimkazi linaloendelea Visiwani humo.

Akimueleza Rais Mwinyi namna atakavyoshirikiana na Bodi ya Maziwa Tanzania na wadau wengine katika kufanikisha kampeni hii, Mkurugenzi wa ASAS Bw. Salim Ahmed amesema kuwa kwa kuanzia wamepanga kugawa zaidi ya lita 5,000 kwenye shule zaidi ya 25 Zanzibar ambapo hatua hiyo imekuja kufuatia ripoti ya mwaka 2022 kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuonesha kuwa asilimia 1.8 ya watoto wa Zanzibar wana tatizo la udumavu jambo lililolazimu kampuni hii kuunga mkono Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni unaoratibiwa na Bodi ya Maziwa Tanzania ili kupunguza na ikiwezekana kumaliza kabisa tatizo hilo.

Ahmed amesema pamoja na hayo, lengo jingine la mpango huo ni kuimarisha lishe na afya za wanafunzi shuleni na wananchi kwa ujumla huku akiwakumbusha kuwa kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu mmoja anatakiwa kunywa maziwa yasiyopungua lita 200 kwa mwaka huku takwimu zikionesha kuwa nchini Tanzania kwa sasa hali ya Unywaji Maziwa siyo yakuridhisha.

Katika uzinduzi huo wa Mpango wa Unywaji Maziwa Shuleni kwa upande wa Zanzibar jumla ya shule tatu za sekondari ya Kizimkazi, Kizimkazi Dimbani pamoja na Hasnu Makame  zilipatiwa Maziwa hata hivyo zoezi la ugawaji maziwa kwa shule nyingine utaendelea Kwa siku tatu mfululizo.